Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Juma Masenza amewataka watendaji wa kata kuhakikisha wanasimamia
kikamilifu suala la ulinzi na usalama katika kata wanazoziongoza, kwa
kuzingatia kuwa hilo ni moja kati ya majumu yao makubwa katika kata zao.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya habari na
mawasiliano ya halmasha ya wilaya ya Mufindi imeeleza kuwa, Mkuuu huyo wa Mkoa
ameyasema hayo wakati wa kikao maalum na
watendaji wa kata 30 za halmashauri
ya wilaya mufindi kilichofanyika mjini Mafinga.
Bi. Masenza amesema, jukumu la kusimamia
maisha na mali za wananchi katika kata wanazoziongoza ni jukumu la msingi kwa
ustawi wa maisha ya watu na taifa kwa ujumla hivyo, linapaswa kupewa kipaumbele
Aidha mkuu huyo wa Mkoa amewahimiza watendaji
hao kujibidisha ili waweze kubaini mipango ya uvunjaji wa amani na usalama kabla
haijatekelezwa kuliko kushughulikia baada ya kufanyika kwa uhalifu hususani unaosababisha
vifo kwa raiya jambo ambalo linakuwa halina maana kwa umma
Awali akitoa mada kuhusu majukumu ya watendaji wa kata, katibu
tawala msaidizi wa serikali za mitaa Mkoa wa Iringa Bw.Wilfred Myuyu, pamoja
na mambo mengine amewataka baadhi ya watendaji wa kata kuacha tabia zinazo
dhalilisha utumishi wa umma zikiwemo za ulevi, uwizi, kutoa siri za serikali
sanjari na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utendaji kazi badala ya
kujifanya miungu watu katika maeneo yao ya kazi.
0 comments:
Post a Comment