Kwa mujibu wa maoni ya msemaji mkuu wa kambi hiyo kwa Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano), Tundu Lissu, tatizo la msingi hapo ni matakwa
ya Sheria ya Kura ya Maoni, 2013.
Alikuwa akiwasilisha maoni ya kambi hiyo bungeni kuhusu mpango na
makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa
mwaka 2015/16.
Alisema sheria hiyo imeweka utaratibu mgumu wa uendeshaji wa kura
ya maoni, ambapo kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa haiwezekani
kuahirishwa wala kuongezewa muda.
“Kwa mfano, ndani ya siku 14 tangu tarehe ya kupokea Katiba
Inayopendekezwa, Rais anatakiwa – kwa amri iliyotangazwa katika Gazeti
la Serikali na baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar – kuielekeza
Tume ya Uchaguzi kuendesha kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa,”
alisema.
Alisema amri ya kura ya maoni inatakiwa kufafanua kipindi cha kampeni na kipindi ambacho kura ya maoni inatakiwa kufanyika.
Alisema Rais Kikwete alikwishatoa amri kwa mujibu wa kifungu cha 4
cha Sheria ya Kura ya Maoni lakini Rais hana mamlaka yoyote, kwa mujibu
wa sheria hiyo ya kutengua amri yake au kutoa amri mpya ili kuwezesha
kura ya maoni kufanyika kwa tarehe nyingine tofauti na tarehe
iliyotangazwa kwenye amri ya kwanza.
Aliongeza ndani ya siku saba baada ya kuchapishwa kwa Katiba
Inayopendekezwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatakiwa kuandaa swali la
kura ya maoni na kulichapisha katika Gazeti la Serikali.
“Na ndani ya siku 14 baada ya kuchapisha swali hilo, Tume inatakiwa
kutoa taarifa ya kufanyika kwa kura ya maoni, itakayoeleza kipindi cha
kuhamasisha na kuelimisha umma juu ya kura hiyo na siku ya kura ya
maoni,” alisema.
Alisema kila msimamizi wa kura anatakiwa ndani ya siku 21 baada ya
kuchapishwa kwa taarifa ya Tume, kuwajulisha wananchi katika jimbo lake
la uchaguzi kuhusu utaratibu wa kufanyika kwa kura ya maoni.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment