Country Fm Iringa 88.5 Iringa,91.1 Mbeya
Home » » Magufuli aendelea kutumbua majipu

Magufuli aendelea kutumbua majipu

RAIS John Magufuli ameendelea kutumbua majipu katika maeneo mbalimbali yenye harufu ya ufisadi, ambapo safari hii ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka kwa ajili ya kupisha uchunguzi dhidi ya matumizi mabaya ya kiasi cha Sh bilioni 13 katika Shirika la Reli Tanzania (TRL).
Pia kutokana na utendaji mbovu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa muda mrefu na hatua kutochukuliwa kudhibiti tatizo hilo, Dk Magufuli ameivunja Bodi yote ya Bandari na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa bodi hiyo, Profesa Joseph Msambichaka na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadh Massawe.
Hii ni mara ya kwanza kwa Dk Magufuli kutengua uteuzi wa kiongozi wa juu wa serikali kama Katibu Mkuu, ikiwa ni mwezi mmoja tangu kuapishwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwinjaka aliteuliwa kushika wadhifa huo wa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na Rais mstaafu Jakaya Kikwete Agosti mwaka 2013, hivyo ameitumikia nafasi hiyo kwa takribani miaka mitatu sasa.
Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko. Mwinjaka atemwa Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kutenguliwa kwa uteuzi wa Dk Mwinjaka, ulitokana na ziara ya ghafla ambayo aliifanya katika shirika hilo la reli.
“Nilifanya ziara ya ghafla TRL ambako katika uchunguzi wa awali nimegundua matumizi mabaya ya fedha Sh bilioni 13 nje ya utaratibu, na kwa sasa uchunguzi unakamilishwa kwa waliohusika. Ila Rais ametengua uteuzi wa Dk Mwinjaka kuanzia leo (jana) na atapangiwa kazi nyingine,” alisema Majaliwa.
Alisema pamoja na ubadhirifu huo, TRL na TPA ni mashirika ambayo yameshindwa kufanya vizuri kwa muda mrefu, ambapo kwa upande wa TRL limeshindwa kabisa kujiendesha.
Alisema Serikali inataka shirika hilo, lijiendeshe lenyewe kwa faida na kutoa huduma stahiki kwa wananchi. Wanane wasimamishwa Pamoja na hayo, Waziri Mkuu alisema amewasimamisha kazi wasimamizi wanane wa Bandari Kavu (ICD) ambao ni Happygod Naftali, Juma Zaar, Steven Naftali Mtui, Titi Ligalwike, Lydia Prosper Kimaro, Mkango Alli, John Elisante pamoja na James Kamwomwa.
Alisema wasimamizi hao, walitajwa kuhusika na upotevu wa makontena takribani 2,387 katika taarifa ya ukaguzi wa ndani ya Julai 30, mwaka huu, ambayo inaonesha TPA iligundua kuwepo kwa vitendo vinavyonesha kuwa bandari hiyo hupitisha makontena mengi bila ya kulipiwa kodi na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa.
 
 Image result for magufuli

Aliwataja viongozi wengine ambao hawakutajwa na taarifa hiyo, lakini ni wahusika wakuu katika sekta zilizotoa ruhusa makontena kutoka ndani ya bandari kuwa ni Shaban Mngazija aliyekuwa Meneja Mapato, Rajab Mdoe Mkurugenzi wa Fedha na Mkuu wa Bandari Kavu, Ibin Masoud Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Apolonia Mosha, Meneja wa Bandari Msaidizi (Fedha).
“Hawa wote nimeagiza wasimamishwe kazi na wawekwe chini ya ulinzi ili kuvisaidia vyombo vya dola wahusika wa makontena hayo waweze kupatikana na hivyo kufanikisha TRA kulipwa kodi yake,” alisisitiza Majaliwa. Mfumo mbovu wa malipo Alisema upotevu huo wa makontena, unaenda sambamba na mfumo usiokidhi wa kupokea malipo unaotoa mwanya mkubwa wa kupoteza mapato ya Serikali.
“Bandari ni eneo muhimu ambako kama itasimamiwa vizuri inaweza kukusanya fedha nyingi na kuchangia pato la taifa. Serikali haitavumilia kuona watu wachache au kikundi chochote kilichojipanga kuhujumu mifumo au kuiibia Serikali kwa namna yoyote ile kwa manufaa ya wachache,” alisema Waziri Mkuu huyo.
Mbali ya Profesa Msambichaka, wajumbe wa Bodi ya TPA iliyovunjwa ni Dk Tulia Ackson, Mhandisi wa Ujenzi, Musa Nyamsingwa, Mtaalamu wa Manunuzi na Mjumbe wa Bodi ya Posta, Donata Mugassa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu.
Wengine ni Mhandisi wa Bodi ya Wahandisi Tanzania, Gema Modu, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Francis Michael, Mkurugenzi wa Mipango NSSF, Crescentius Magori na aliyekuwa Mkurugenzi wa Masoko wa TPA, Flavian Kinunda. Bodi hiyo iliteuliwa Juni mwaka huu na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu Majaliwa alifanya ziara za kushtukiza katika shirika la TRL na TPA, ambapo akiwa bandarini, alikagua mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo na utozaji wa malipo baada ya kupewa taarifa kwamba kuna makontena 2,431 yametolewa bila kulipiwa ushuru.
Baada ya kuibua madudu hayo, alimtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Hebel Mhanga ampelekee majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi huo na kutoa wiki moja kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo, inabadilisha mfumo wa utozaji malipo na kuweka mfumo wa malipo wa kielektroniki.
Alipotembelea TRL, alikagua mabehewa na kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye stesheni hiyo, ambako alibaini madudu kwenye malipo ya mishahara na makato ya michango ya wafanyakazi.
Aidha alibainisha kuwa anazo taarifa za shirika hilo kupewa fedha na Serikali kiasi cha Sh bilioni 13.5 kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya reli, lakini halikufanya hivyo.
Ahsante kwa maoni yako,endelea kusikiliza redio country fm Iringa-One community
Facebook Blogger Plugin: Bloggerized by Joseph Kipangula Enhanced by Joseph Kipangula

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA COUNTRY FM

Pages

Pages

radio country fm,one community. Powered by Blogger.