Country Fm Iringa 88.5 Iringa,91.1 Mbeya
Home » » HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WAKUU WA WILAYA

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WAKUU WA WILAYA

Namshukuru Waziri Mkuu kwa kunialika na kunishirikisha katika ufunguzi wa Mafunzo ya Wakuu wa Wilaya Wapya.   

Nakupongeza Waziri Hawa Ghasia na uongozi wa TAMISEMI kwa kuandaa mafunzo haya muhimu kwa ajili ya viongozi wetu muhimu sana katika safu ya uongozi wa nchi yetu. 

Nawapongeza pia kwa kuchagua mahala pazuri na tulivu pa kuendeshea mafunzo haya.     


Hii siyo mara ya kwanza kuwa na mafunzo ya namna hii, tumekuwa tukifanya hivi kila tunapofanya mabadiliko ya uongozi katika ngazi mbalimbali ili kupata fursa ya kuelekezana kuhusu wajibu na majukumu ya kazi za viongozi wa Serikali katika maeneo yao.  Nawapongeza kwa kudumisha utaratibu huu mzuri.  

Pongezi kwa Uteuzi
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;

Napenda kutumia nafasi hii kwa mara nyingine tena kuwapongeza wote kwa kuteuliwa kwenu kuwa Wakuu wa Wilaya. Nimewateua kwa sababu nimeridhika kuwa mmekidhi sifa na vigezo vya kuweza kumudu majukumu niliyowapa ya kuongoza Wilaya.  Nendeni mkachape kazi ili mkidhi matarajio yangu kwenu  na ya wananchi mtakawaongoza.    Nimewaamini, naomba mkalipe imani  yangu kwenu kwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa uadilifu na uaminifu. 
Madhumuni ya Semina
Ndugu Viongozi;
Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, lengo la mafunzo haya ni kuwapatia stadi na maarifa mahsusi yatakayowawezesha kutekeleza wajibu na majukumu yenu ya Ukuu wa Wilaya kwa ufanisi.  Nimeona ratiba yenu na mada 11 zilizoandaliwa na watu waliobobea katika masuala ya uongozi na utawala.  Nafurahi kwamba kuna fursa ya majadiliano baada ya kila somo kutolewa. Bila ya shaka mwisho wa mafunzo haya mtakuwa mmepata miongozo mahususi  kuhusu majukumu yenu, wajibu wenu na  utendaji kazi wenu. Naamini mtarejea vituoni kwenu mkiwa  mmeiva vya kutosha na kwamba mkizingatia mlichofundishwa,  mkiongeza na uzoefu wenu na mkiwa wabunifu mnaweza kufanya maajabu. Mtatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi wa hali ya juu na kushangaza wengi. 
Wajibu wa Mkuu wa Wilaya
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Mkuu wa Wilaya ndiye kiongozi mkuu wa Serikali katika Wilaya. Ndiye mwakilishi wa Rais katika Wilaya. Hakuna mwingine. Ndiye mhimili wa shughuli za Serikali Wilayani.  Ni dhamana kubwa hivyo ni lazima mfanane nayo katika utendaji wenu, wa kasi na katika maisha yenu ya kila siku ofisini katika jamii na hata nyumbani.  Lazima muwe mfano kwa tabia njema kwa kauli na matendo yenu. Muwe na nidhamu ya hali ya juu na uadilifu usiotiliwa shaka. Wapo wenzenu tuliowaondoa  kwa kukosa sifa hizo. Lazima wakati wote mzingatie matakwa ya Katiba, Sheria na taratibu za nchi ndiyo utawala bora.
 Kama mjuavyo na kama hamjui naamini katika mafunzo haya mtajua kwamba Serikali ina majukumu ya namna tatu.  Kwanza, ina jukumu la utawala, pili, ina jukumu la usalama na tatu, ina jukumu la maendeleo.  Hivyo basi, Mkuu wa Wilaya nae kama kiongozi mkuu wa Serikali katika eneo lake wajibu wake nao umegawanyika pande hizo tatu.
Jukumu la kiutawala la Mkuu wa Wilaya ni lile la kuhakikisha kwamba mifumo ya utawala katika wilaya yake inafanya kazi  vizuri na kwa ufanisi.  Mambo yote  yanakwenda vizuri, sheria zinafuatwa kanuni na taratibu zinazingatiwa na haki inatekelezwa katika Wilaya yake.  Hakuna jambo ambalo halihusu Serikali: ya Kiserikali yanaihusu Serikali na ya jamii na ya watu binafsi nayo pia yanaihusu Serikali. Ninaposema hivyo sina maana kuwa Mkuu wa Wilaya anafanya kila  kitu au anatoa maelekezo kwa kila jambo linalofanywa na kila taasisi na kila mtu katika Wilaya yake. Hapana. Kila jambo lina mtu wake anayehusika nalo na wengi wa watu hao hawawajibiki kumhusisha Mkuu wa Wilaya au Serikali.  Ni wajibu wako kujua nani anahusika na lipi, ili uweze kuhakikisha kwamba majukumu hayo yanatekelezwa ipasavyo. 
Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kuwa hata mambo binafsi ya jamii na raia yanafanyika vizuri, kwa ufanisi na kwa kufuata sheria.  Hii ina maana kuwa zaidi ya kujua vizuri shughuli za Serikali Kuu na Halmashauri ya Wilaya na Serikali za Mitaa, ni lazima pia ajue vizuri mila na desturi za jamii na maisha ya watu waliopo katika Wilaya yake na ahakikishe kuwa mambo yao yanakwenda vizuri.  Kuwafanya watu wetu wawe na furaha ni wajibu wa msingi wa Serikali.
Hamna budi kutambua kwamba mfumo wa utawala wa Serikali Kuu unaishia kwenye tarafa.  Lakini pia mjue kwamba yapo madaraka ya utawala na ulinzi wa amani yaliyogatuliwa kwa Makatibu Kata.  Watumieni viongozi hao katika kutekeleza majukumu yenu.  Hata hivyo, hamna budi kuhakikisha kwamba wanayatumia madaraka haya vizuri na kwa ufanisi. 
Kwa upande wa jukumu la usalama, Serikali inawajibu wa kuhakikisha kuwa kuna amani na utulivu na kuna usalama wa maisha ya watu, mali zao na rasilimali za taifa. Kwa ajili hiyo Mkuu wa Wilaya anakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kama Mkuu wa Mkoa alivyo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Rais ni Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Taifa.
Nimeona kuwa mtafundishwa kuhusu Kamati ya Ulinzi na  Usalama ya Wilaya na wajibu wenu.  Kamati hiyo ndiyo yenye dhamana ya kumshauri, kumsaidia na kumuwezesha Mkuu wa Wilaya kutimiza ipasavyo majukumu ya kiusalama ya Serikali katika Wilaya.  Ni wajibu wa Mkuu wa Wilaya kuhakikisha kuwa Kamati hii inakutana kwa mujibu wa kanuni zake. Kamati hii ikitimiza ipasavyo wajibu wake matukio yote ya kiusalama yataweza kuyashughulikiwa vizuri.  Hali kadhalika, matishio au viashiria vya kuhatarisha usalama vitatambuliwa mapema na hatua zipasazo kuchukuliwa.
Kwa namna hiyo basi Mkuu wa Wilaya anaweza  kuhakikisha kuwa Wilaya yake itakuwa salama na watu watapata nafasi ya kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo katika mazingira salama na tulivu. Wakuu wote wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vilivyopo Wilayani ni wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama anayoiongoza Mkuu wa Wilaya.  Ni vyema Mkuu wa Wilaya akatambua  kwamba vyombo hivyo vina uhuru wake katika kufanya shughuli na haviwajibiki  moja kwa moja kwake kwa kila jambo.  Vina wajibu kwa wakuu wa vyombo walio juu yao, walioko nje ya Wilaya. Hata taarifa zao huzipeleka  huko ingawaje wanaweza kumuambia Mkuu wa Wilaya  yale yahusuyo Wilaya yake ambayo wanaona anayowajibika kujua.  Naomba mzifahamu vizuri taratibu hizo za vyombo kufanya kazi zake ili muepushe migongano isiyokuwa ya lazima muweze kuvitumia kwa ufanisi mzuri zaidi. Mkiyafahamu vizuri yote haya mtavitumia vyombo hivyo bila kuvunja taratibu zake na bila mikwaruzano. Mtajihakikishia mafanikio makubwa.
Jukumu la tatu la Serikali na hivyo la Mkuu wa Wilaya ni la kuwaletea maendeleo wananchi.  Hapa kuna mambo mawili. Upande mmoja Serikali inalo jukumu la moja kwa moja la kupanga mipango ya maendeleo na kuitekeleza.  Upande wa pili, Serikali ina wajibu wa kuwasaidia wananchi kujiletea maendeleo kwa kuwapa ushauri au kuwaongezea nguvu kwa yale wafanyayo.
Kwa mujibu wa mfumo wetu wa utawala ulivyo, shughuli za maendeleo zinapangwa na kutekelezwa na Halmashauri za Wilaya na Miji. Hivyo basi, Mkuu wa Wilaya hahusiki moja kwa moja na upangaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika Wilaya.  Namna bora ya kuweza kufanya hivyo ni kuwa na uhusiano wa karibu na viongozi wa Halmashauri na hasa kuwa vikao vya mashauriano.  Kupitia vikao hivyo mnaweza kuelewana juu ya mambo ambayo Halmashauri itayaingiza katika mipango na programu zake.  Mkuu wa Wilaya anaweza kutumia DCC ingawaje inafanyika mambo yamekwisha kamilika. Hata hivyo, analo jukumu la kusimamia utekelezaji wa mipango hiyo inayofanywa na Halmashauri zake. Mkuu wa Wilaya anategemewa kufanya ziara za mara kwa mara katika Wilaya yake kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli mbalimbali zifanywazo na Serikali Kuu, Halmashauri na wananchi.
Mkuu wa Wilaya anapaswa kuwa mhamasishaji mkuu wa maendeleo katika Wilaya yake. Wakuu wa Wilaya wana jukumu la msingi la kuhakikisha shughuli zote za kiuchumi na miradi ya maendeleo zinatekelezwa ipasavyo kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.  Hivyo basi, mnapaswa pia kuelewa mipango yote ya maendeleo kwenye maeneo yenu pamoja na shughuli zote za kiuchumi zinazofanywa na Serikali Kuu, Halmashauri, taasisi na watu bianafsi kuhakikisha hazikwami.   Hali kadhalika, hamna budi kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za umma.  Ama kwa kujitolea nguvu zao au kwa kuchangia kwa hiari na kutoa kodi na tozo stahili.  Shirikianeni kwa karibu na Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri na Madiwani ili kujenga ushirikiano na maelewano katika utendaji wa kazi. 
Ili muweze kutekeleza majukumu yenu ya maendeleo ni  wajibu wenu kuhakikisha kuwa hamkai ofisini muda wote.  Lazima mtoke kwenda kukagua shughuli za maendeleo na kukutana na kuzungumza na wananchi.
Tumewateua mkawatumikie wananchi na si vinginevyo.  Hatukuwateua mkakae ofisini tu, wafuateni wananchi waliko, mkasikilize shida na kero zao na mkazitafutie majawabu. Yale yatakayowashinda wapelekeeni viongozi wa juu yenu.  Tumewateua mkawe wakombozi wa matatizo yao, tumewateua mkawe daraja la kupita kuelekea kwenye maendeleo.  Kafanyeni kazi. 
Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema kwamba: “Kiongozi mzuri katika Taifa letu, ni yule anayekerwa na matatizo ya wananchi”.  Maneno haya ya busara bado ni muhimu hata sasa. Jukumu kubwa tunalotakiwa kujishughulisha nalo ni kutatua kero na matatizo ya watu.  Mnategemewa muonekane hivyo kwa kauli zenu, mienendo yenu na matendo yenu.  Watu lazima wayaone matumaini ya kupata majawabu ya changamoto zao kupitia kwenu.  Wanapaswa kuwaona kuwa ninyi ndiyo kimbilio lao.  Mnategemewa kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowakabili na katu msiwe sehemu ya matatizo au wanung’unikaji.
Mahusiano ya Mkuu wa Wilaya na Wadau wengine
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Mkuu wa Wilaya pia ni kiungo kati ya Serikali Kuu na wadau wengine katika nyanja mbalimbali za maisha ya Watanzania, kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kiusalama. Ninyi kama viongozi wakuu wilayani mna wajibu wa kujenga mahusiano mazuri na vyama vyote vya siasa vilivyo katika maeneo yenu pamoja na viongozi na taasisi za dini, viongozi wa kijamii na asasi zisizokuwa za kiserikali.  Mkijenga uhusiano mwema na makundi hayo itasaidia sana utekelezaji wa mambo mengi muhimu ya maendeleo ya watu na mtaweza kuepuka migogoro ya kisiasa na kijamii inayoweza kujitokeza katika maeneo yenu. 
Ni vyema mkatambua kuwa viongozi wa dini na wa kijamii wana mchango muhimu katika ustawi na maendeleo ya maeneo yenu ya uongozi. Wananchi wanawasikiliza, hivyo basi mkiwa na mahusiano mema nao, itakuwa rahisi kwa mambo mengi kutekelezeka hata yale ambayo yanaweza kuonekana kuwa huenda yangekuwa magumu. Pia, viongozi hawa ni tegemeo kubwa  katika kudumisha amani na utulivu nchini na kusaidia katika huduma mbalimbali za jamii.  Hivyo jengeni uhusiano mzuri na viongozi hawa. 
Ndugu Viongozi;
Wakuu wa Wilaya wana uhusiano maalum na chama Tawala kama ilivyo kwangu, kwa Waziri Mkuu na kwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.  Serikali hii ni ya Chama cha Mapinduzi kilichoshinda uchaguzi.  Inatekeleza Ilani ya Uchagui ya CCM, hivyo tunao wajibu wa kutoa tarifa ya mara kwa mara kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa Ilani na majukumu mbalimbali ya Serikali.  Mkuu wa Wilaya anao wajibu huo kwa Chama katika Wilaya yake.  Ni lazima afanye hivyo katika vikao husika vya Chama vya Wilaya. Si jambo la hiari wala si jambo la muhari unapotakiwa kufanya hivyo.  
Majukumu Maalumu ya Kitaifa
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Kila wakati una mambo yake muhimu kitaifa ambayo hamna budi kuyashughulikia.  Wakati huu pia una mambo yake.  Napenda kuyataja baadhi. Jambo la kwanza, ni ujenzi wa maabara za sayansi katika Sekondari za Kata.  Nilitoa agizo Novemba 2012, kuwa kila shule ya sekondari ya kata ambayo haina maabara za masomo ya ya sayansi ziwe nazo ifikapo Novemba, 2014.  Kazi kubwa na nzuri imefanyika na takribani kila Wilaya Maabara nyingi zimejengwa.  Kwa kutambua kasi iliyokuwa inaendelea niliongeza muda mpaka Juni, 2015 wa kumalizia ujenzi paliposalia.  Sitaki maelezo kuwa hukuwepo.  Utakuwa umeshindwa kazi.  
Jambo la pili, uboreshaji wa daftari la wapiga kura. Kama mjuavyo zoezi la uandikishaji wa wapiga kura limeshaanza katika mkoa wa Njombe na litaendelea katika mikoa mingine kwa mujibu wa ratiba ya Tume.  Jihusisheni kwa ukamilifu katika kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Wakumbusheni wananchi kwamba kuwa na kitambulisho cha mpiga kura ndiko kutawawezesha wao kushiriki katika zoezi la upigaji wa Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu baadae Oktoba, 2015.  Haipo fursa nyingine.
Jambo la tatu, ni Kura ya Maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanashiriki kwa ukamilifu bila kukosa  katika mchakato huo. Ndiyo maana ninawataka muwahimize wananchi wajiandikishe na pia washiriki wakati wa zoezi la kutoa elimu kwa umma na kampeni kabla ya Kura ya Maoni. Hakikisheni  wakati wote wa  zoezi la upigaji kura kuna amani na utulivu.  Tumieni vizuri mamlaka yenu ya ulinzi wa amani katika maeneo yenu ili wananchi waelimishwe, kampeni zifanyike  na wananchi wapige kura kwa amani na salama.  Tunataka wananchi wapate fursa ya kuamua wanavyoona inafaa kwa uhuru.  
Jambo la nne, ni kuhusu Uchaguzi Mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Kama mjuavyo tunatarajia kuwa na Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba, 2015. Ninyi kama Viongozi mna wajibu wa kuhakikisha kuwa uchaguzi huu unafanyika katika hali ya utulivu na amani na kila mwananchi anashiriki kwa uhuru katika uchaguzi huo. Hamasisheni wananchi wa maeneo yenu wajiandikishe katika daftari la kudumu la wapiga kura hivi sasa ili waweze kuitumia haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Zipo  changamoto kadhaa za kitaifa ambazo hamna budi kuziwekea mikakati maalum ya kuzitafutia uamuzi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Nitazitaja kwa kifupi nikitumaini kuwa baadhi huenda zikazungumzwa katika mafunzo au mtazikuta Wilayani kwenu na waliowatangulia watawasaidia kuwafafanulia.  Tunachotegemea kutoka kwenu ni kuwa na mikakati na mipango thabiti ya kutafuta majawabu.  Mambo haya ni pamoja na:
(i)                Wimbi la Wahamiaji haramu na wavamizi katika misitu ya Hifadhi.  Tatizo hilo lipo  zaidi katika Mikoa ya Mipakani;
(ii)             Lipo tatizo kubwa la biashara na matumizi ya dawa za kulevya, ambalo limesababisha madhara makubwa, hasa kwa Vijana na kuivuruga sifa nzuri ya nchi yetu. Lazima tufanye kila tuwezalo tuzuie na kuikomesha.
(iii)          Ipo migogoro ya ardhi katika maeneo mengi nchini ambayo mingi inasababishwa na baadhi ya Watendaji kwa kutozingatia ipasavyo maadili ya kazi zao. Tufanye kila tuwezalo tuitafutie jawabu.
(iv)          Kuna migogoro ya wakulima na wafugaji katika sehemu nyingi nchini ambayo tunawajibika kuingilia kati mapema kuzuia isilete maafa.  Na lililo muhimu zaidi ni kuipatia ufumbuzi wa kudumu kwa kupanga matumizi bora ya ardhi na kugawa maeneo ya kilimo  mbali ya ufugaji na kusimamia mpango huo.
(v)            Kuna tatizo kubwa la ujangili wa wanyama pori hasa ndovu, faru, simba na chui ambalo hatuna budi kulikomesha. Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya zishirikiane na wadau kupambana na uhalifu huu.
Hayo ni baadhi ya masuala muhimu kitaifa lakini kila Wilaya ina mambo yake.  Naomba muende mkashirikiane na viongozi wenzenu na wananchi kubaini matatizo maalum ya maendeleo katika maeneo  yenu na kubuni mikakati wa kuyatatua.
Hitimisho
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Naomba nimalize kwa kuwatakia mafunzo mema na utekelezaji mwema wa wajibu na majukumu yenu baada ya mafunzo haya kuhitimishwa.  Nendeni mkafanye kazi kwa ubunifu mkubwa, kwa juhudi na maarifa ili muwasaidie wananchi walio katika maeneo yenu kuondokana na umaskini.  Hivyo, ni muhimu kila mmoja akatimiza wajibu wake kwa ukamilifu.
Baada ya kusema hayo napenda kutamka kuwa, mafunzo haya ya Wakuu wa Wilaya yamefunguliwa rasmi.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

Ahsante kwa maoni yako,endelea kusikiliza redio country fm Iringa-One community
Facebook Blogger Plugin: Bloggerized by Joseph Kipangula Enhanced by Joseph Kipangula

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA COUNTRY FM

Pages

Pages

radio country fm,one community. Powered by Blogger.